Na Paul Kayanda,Bukombe
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umetoa mafunzo kuhusu matumizi ya nishati safi kwa Taasisi ya Maendeleo ya Viziwi Tanzania (TAMAVITA) wilayani Bukombe, mkoani Geita.
Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Mhandisi, Kelvin Tarimo alisema hayo juzi wakati akitoa mafunzo hayo wilayani Bukombe Mkoani Geita kwa kushirikiana na maafisa maendelelo ya jamii wa halmashauri hiyo sambamba na ofisi ya mkuu wa wilaya kuendesha zoezi la ugawaji wa majiko ya gesi kwa makundi maalumu yaliyojumuisha ealemavi wa kudikia, walemavu wa ngozi pamoja na walemavu wa viungo.
Aidha Mhandisi Kelvin Tarimo alisema Mafunzo hayo yanalenga kuhamasisha matumizi bora ya nishati safi ya kupikia ili kusaidia jamii ya viziwi kupata uelewa kuhusu faida za matumizi ya nishati safi ya kupikia na endelevu katika kuboresha maisha yao.
"REA inahakikisha kuwa jamii zote, ikiwemo watu wenye ulemavu, wanapata fursa sawa ya kutumia nishati safi na kuleta mabadiliko chanya katika maisha yao,"alisema Mhandisi Kelvin Tarimo
Naye katibu Tawala wa Wilaya ya Bukombe, Ali Mketo akigawa majiko ya gesi kwa makundi hayo alieleza kusikitishwa na kundi hilo kutochangamkia fursa ya mikopo ya halmashauri na kwamba mpaka sasa fedha ipo na ni haki yao ya msingi.
Maketo alisisitiza kwamba halmashauri ina fedha za mikopo ambazo zimekusudiwa kusaidia makundi maalum, ikiwemo watu wenye ulemavu, lakini wengi wao hawachangamkii fursa hiyo na hawajachukua haki yao.
Liongozi huyo alisema kuwa mikopo hii ni muhimu kwa kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu, kwani inaweza kuwasaidia kuanzisha au kuboresha shughuli zao za kiuchumi, lakini hali ya kutokuchukua mikopo hiyo inahatarisha juhudi za halmashauri katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.
"Ni muhimu kwa watu wenye ulemavu kuchukua mikopo hii kwa sababu halmashauri inatoa fedha ambazo zinahitaji kuchukuliwa ili kutumika katika kuboresha maisha yao. Tumeshuhudia hali ya chini ya watu hawa kujiunga na mikopo hii, jambo linaloweza kudhoofisha juhudi za kuboresha maisha yao," alisema Mketo.
Aliendelea kusema kuwa mikopo hiyo inatolewa kwa masharti rahisi na ni fursa nzuri kwa watu wenye ulemavu, hasa ikizingatiwa kuwa inawapa nafasi ya kutekeleza miradi ya kiuchumi inayoweza kuwasaidia kujikimu na kuboresha ustawi wao.
Mketo alitoa wito kwa watu wenye ulemavu wilayani Bukombe kuchangamkia mikopo hiyo na kuwaasa kutumia fursa hii vizuri ili kujenga uchumi wa familia zao na jamii kwa ujumla.
Alisema kwamba halmashauri itaendelea kutoa elimu na msaada kwa watu wenye ulemavu kuhusu jinsi ya kupata mikopo hii, ili kuhakikisha kuwa wanachangia katika maendeleo ya wilaya yao.
Mikopo ya halmashauri, ambayo imekuwa ikitolewa kwa makundi maalum, ni mojawapo ya mikakati ya serikali ya wilaya ya Bukombe kusaidia watu wa rika na makundi mbalimbali kukuza uchumi wao na kupunguza umasikini.
Rosemary John, ni Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona Wilaya ya Bukombe, ambapo kwa niaba ya wenzake alilishukuru REA Mamlaka ya Nishati ya Vijijini Rea kwa kuwapa mafunzo ya ufanisi kwa watu wasioona na kwamba mafunzo hayo yamewawezesha kupata ujuzi muhimu katika nyanja mbalimbali.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukombe, kwa niaba ya ofisi ya mkuu wa wilaya, aliwagawia wasioona majiko ya gesi kama sehemu ya juhudi za kuboresha maisha yao na kupunguza utegemezi wa nishati ya kuni, hasa katika maeneo ya vijijini. Huu ni mchango mkubwa katika kukuza ustawi wa jamii na kuongeza fursa kwa watu wasioona.









