Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda amechukua hatua za haraka kutatua changamoto ya miundombinu katika kata ya Mhongolo Manispaa ya Kahama, kufuatia kero zilizowasilishwa na vijana wakati wa sherehe za Krismasi walipokutana naye kwa chakula cha pamoja (Pilau la Wana).
Leo Desemba 31, 2025, DC Nkinda ametembelea Mtaa wa Mhongolo ambapo amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13, akiwataka watumishi wa umma kuwahudumia wananchi kwa vitendo na kuwaletea tabasamu wale waliomwamini na kumpa ridhaa ya kuwaongoza.
Akizungumza na waandishi wa habari, Nkinda amesema Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama imefanikiwa kutafuta mtambo wa kuchonga barabara (greda) ili kuanza kushughulikia kero za barabara zilizoharibika katika maeneo mengi kutokana na mvua, akisisitiza kuwa lengo ni kuhakikisha wananchi hawakwami katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyashimbi, Kata ya Mhongolo, Emanuel Lutonja, amemshukuru Rais Samia pamoja na DC Nkinda kwa hatua hiyo, akisema ujio wa greda katika mtaa wake umepunguza kwa kiasi kikubwa kero za barabara zilizokuwa na madimbwi makubwa yaliyowaathiri wafanyabiashara, hususan bodaboda, bajaji na wajasiriamali walioko pembezoni mwa barabara.
Mkazi wa Nyashimbi Sokoni, Japhet Kitima, amesema awali wafanyabiashara walipata changamoto kubwa kuingiza mizigo kwa magari kutokana na ubovu wa barabara, hali iliyosababisha hasara hivyo wanamshukuru DC kwa kuwaletea greda kwani sasa hali imeanza kubadilika.
Katika ziara hiyo, DC Nkinda ametembelea barabara ya Mhongolo Senta kuelekea KACU pamoja na barabara ya Mhongolo kuelekea Nyashimbi Sokoni, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushughulikia kero za wananchi kwa vitendo na kwa wakati.