Na Samuel Samsoni Kahama
MKUU wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Frank Nkinda, amekutana na makundi mbalimbali ya vijana wilayani humo katika hafla ya pamoja ya kusherehekea Sikukuu ya Krismasi, iliyolenga kuimarisha mshikamano kwa kula chakula cha pamoja sambamba na kusikiliza changamoto zinazowakabili vijana wa Kahama.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo wilayani Kahama, Abas Omari, ameomba kuwekwa taa za barabarani katika eneo la Shunu ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za kibiashara nyakati za usiku, kutatua changamoto ya barabara ya kuelekea makaburini ya Shunu ambayo huwa haipitiki wakati wa mvua kutokana na tope, hali inayowalazimu baadhi ya wananchi, wakiwemo waliovaa kanzu, kuzikunja ili kupita.
Akitoa nasaha zake, Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya ya Kahama (OCD), Mtaju, amewataka wananchi na vijana kutokuwa na hofu ya kufikisha changamoto zao polisi wakati wowote Pia, amewahimiza vijana kutumia hekima katika kutatua changamoto zinazowakabili.
Akijibu hoja na kero zilizowasilishwa, Nkinda amesema kuhusu barabara ya makaburini Shunu, ameahidi kutatua changamoto hiyo ndani ya muda mfupi akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina utaratibu wa kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi, iwe ni kwa makundi au mtu mmoja mmoja, akibainisha kuwa milango ya ofisi yake iko wazi kwa wananchi wote.
Katika hitimisho lake, Mkuu wa Wilaya amewataka vijana wa Kahama kuendelea kuwa watulivu, kulinda amani na mshikamano, akisisitiza kuwa uongozi wa wilaya uko pamoja nao katika kuhakikisha maendeleo na ustawi wa wananchi wa Kahama yanaendelea kupatikana.
