Serikali kuchukua Hatua za Kisheria Mkandarasi wa Barabara za Mradi wa TACTIC Kahama | NEWS PLANET

Thursday, January 15, 2026

Serikali kuchukua Hatua za Kisheria Mkandarasi wa Barabara za Mradi wa TACTIC Kahama

  Sammy Media       Thursday, January 15, 2026




Serikali imesema iko tayari kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mkandarasi Sichuan Road and Bridge Group (SRBG) anayetekeleza ujenzi wa barabara na mifereji ya maji katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, kufuatia utekelezaji usioridhisha na ukiukwaji wa masharti ya mkataba.

Akizungumza jana Januari 15, 2026, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Miundombinu katika Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Rogatus Matilila, amesema kasi ya utekelezaji wa mradi huo hairidhishi licha ya mkandarasi kuongezewa muda mara kadhaa.

Kauli hiyo imetolewa wakati wa ziara ya ukaguzi na tathmini ya mradi huo, ambapo Matilila aliambatana na timu ya wataalamu kutoka TAMISEMI wanaosimamia miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miji Tanzania (TACTIC).

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa mradi, Samuel Mtawa, amekiri kuwepo kwa ucheleweshaji mkubwa wa utekelezaji wa kazi, akieleza kuwa hadi sasa mkandarasi ameweza kuweka lami kwa urefu wa kilomita moja tu kati ya kilomita 12 zilizopangwa, pamoja na ujenzi wa mitaro katika baadhi ya maeneo ya mji.

Matilila amesema kuwa muda wa mwisho wa nyongeza ya siku 230 aliyopewa mkandarasi huyo unaishia kesho Januari 15, 2026, huku mkandarasi akiendelea kuwasilisha maombi ya nyongeza zaidi ya muda.

“Maendeleo ya kazi kwa mkandarasi huyu siyo ya kuridhisha kabisa. Ameongezewa muda mara nyingi lakini mpaka sasa yuko nyuma sana. Tayari ameshakatwa fidia hadi asilimia 100, lakini bado anaomba kuongezewa muda tena,” amesema Matilila.

Ameongeza kuwa, licha ya mkandarasi huyo kulipwa zaidi ya asilimia 20 ya thamani ya mkataba, utekelezaji wa ujenzi wa barabara na mifereji ya maji ya mvua bado ni wa kusuasua.

“Leo ndiyo mwisho wa muda wa nyongeza, hivyo tutakaa kama timu kupitia ripoti za mradi na masharti ya mkataba ili kufanya uamuzi sahihi; ama kuendelea na mkandarasi huyu au kuvunja mkataba na kumpata mkandarasi mwingine, kwa lengo la kuwaondolea wananchi adha wanayoipata,” amesisitiza.

Kwa mujibu wa Matilila, sababu zinazotolewa na mkandarasi kujitetea—ikiwemo mvua, uwepo wa maji katika eneo la mradi na changamoto ya upatikanaji wa lami—ni za kujirudia na hazina uzito wa kutosha.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, amekiri kuwepo kwa ucheleweshaji mkubwa wa mradi huo, hali inayowaathiri wananchi hususan wakati wa msimu wa mvua.

“Kama Halmashauri na mwajiri wa mkandarasi, haturidhishwi na kasi ya utekelezaji wa mradi huu. Mpaka sasa kilomita moja tu ya lami imewekwa kati ya kilomita 12 zilizopangwa,” amesema Kibetu.

Wananchi wa Manispaa ya Kahama nao wameeleza kuchoshwa na hali hiyo. Mkazi wa Kahama, Sofia Mbacha, akizungumza katika mkutano wa hadhara ulioongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, ameomba serikali ichukue hatua kali dhidi ya mkandarasi huyo.

“Mitaro waliyochimba ni mikubwa sana. Mvua ikinyesha tunaishi kwa hofu, nyumba zinaweka nyufa na nyingine zinaanguka. Kama huna uwezo wa kuzuia maji kwa mifuko ya moramu unaumia. Kazi zinafanywa kwa mwendo wa kinyonga,” amesema Sofia.

Hatua zitakazochukuliwa na serikali dhidi ya mkandarasi huyo zinatarajiwa kutoa mwelekeo mpya wa utekelezaji wa mradi huo muhimu, unaolenga kuboresha miundombinu na maisha ya wakazi wa Manispaa ya Kahama.




logoblog
Previous
« Prev Post