TISEZA Yatajwa Kuwa Injini ya Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 | NEWS PLANET

Wednesday, February 4, 2026

TISEZA Yatajwa Kuwa Injini ya Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

  Sammy Media       Wednesday, February 4, 2026





Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) ni nguzo muhimu katika kutafsiri na kutekeleza maono, ndoto na matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika sekta ya uwekezaji.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Uwekezaji la Kanda ya Ziwa lililoandaliwa na TISEZA jijini Mwanza, Mhe. Kapinga alisema jukumu la Serikali na Taifa kwa ujumla ni kuwa na maono makubwa ya maendeleo, huku TISEZA ikipewa dhamana ya kuyageuza maono hayo kuwa vitendo vinavyoleta maendeleo ya kweli na endelevu kwa Watanzania.

Alieleza kuwa kupitia majukumu yake ya kuratibu, kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji nchini pamoja na kuendeleza maeneo maalum ya kiuchumi, TISEZA imekuwa chombo muhimu katika kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Mhe. Kapinga alibainisha kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi tatu bora barani Afrika katika kuvutia uwekezaji na kuwa na mazingira bora ya kufanya biashara ifikapo mwaka 2050.

Amesisitiza kuwa kufanikisha azma hiyo kunahitaji ushirikiano wa karibu kati ya TISEZA, Sekta Binafsi na Serikali kwa ujumla kupitia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ikiwemo MKUMBI II.

Aidha, Waziri Kapinga aliitaka TISEZA kufanya kazi kwa karibu na Sekretarieti za Mikoa yote nchini pamoja na Sekta Binafsi, ili kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika fursa za uwekezaji, iwe ni kupitia miradi binafsi au ubia na wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.









logoblog
Previous
« Prev Post