Polisi Mkoa wa Mara inawashikilia watu wanne kwa tuhuma za kuiba gari la wagonjwa (ambulance) kisha kulibadilisha na kuwa gari la biashara ya kubeba watalii.
Watuhumiwa hao wakazi wa Tarime mkoani Mara na jijini Arusha wanatuhumiwa kuiba gari hilo mali ya Halmashauri ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara iliyokuwa ikitoa huduma hospitali ya manispaa hiyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amesema kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari Februari 3, 2026 kuwa gari hilo liliibwa Oktoba 25, 2025 likiwa limeegeshwa kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma mita chache kutoka ilipo hospitali ya manispaa hiyo.
"Baada ya kupata taarifa tulianza uchunguzi na upelelezi na katika uchunguzi wetu tulikamata watu wengi wakiwamo watumishi wa Serikali, lakini baada ya uchunguzi tumebaini kuwa wahusika ni hawa wanne tuliobaki nao," amesema.
Hata hivyo, Kamanda Lutumo hakuwa tayari kutaja kazi za watuhumiwa hao kwa madai kufanya hivyo kutavuruga masuala mengine kwenye kesi hiyo. Taarifa zinadai miongoni mwa watuhumiwa hao wapo pia watumishi wa Serikali.
